(ABNA24.com) Meli hiyo ilikumbwa na mlipuko katika umbali wa maili 60 kutoka bandari wa Jeddah huko Saudi Arabia na baadhi ya mafuta yake yamevuja baharini. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Muosavi ametoa radiamali kwa shambulio dhidi ya meli hiyo ya mafuta ya Iran katika Bahari Nyekundu akisema: Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Mafuta la Taifa la Iran unaonyesha kuwa, meli hiyo ilishambuliwa mara mbili katika muda uliopishana kwa karibu nusu saa katika eneo la kaskazini mwa Bahari Nyekundu.
Katika miezi kadhaa iliyopita pia, kulifanyika vitendo nyingine vya uharibifu dhidi ya meli za mafuta za Iran katika Bahari Nyekundu na uchunguzi unaendelea kufanywa ili kutambua wahusika wa matukio hayo na lile la Ijumaa iliyopita. Radiamali mbalimbali zimetolewa na vyombo vya habari na baadhi ya nchi zikiwemo Russia na China kuhusu kushambuliwa meli ya mafuta ya Iran katika Bahari Nyekundu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitahadharisha kwamba, kuna pande za kikanda na nje ya eneo la Ghuba ya Uajemi zinazotekeleza njama ya kuvuruga usalama na kuzusha machafuko katika eneo hilo.
Diako Hosseini Mkurugenzi wa World Studies Program katika Kituo cha Mafunzo ya Kistratejia chenye makao yake hapa Tehran ameashiria mashambulizi yaliyolenga meli mbili za mafuta katika Bahari ya Oman wiki kadhaa tu baada ya mashambulizi kama hayo dhidi ya meli moja ya mafuta katika bandari ya al Fujaira karibu na pwani ya Imarati na kutaja pande zinazotajwa kuhusika katika mashambulizi hayo.
Mashambulizi ya kigaidi dhidi ya safari za meli baharini yanaweza kuwa na taathira kubwa mbaya. Hata hivyo mapendekezo yaliyotolewa wa Wamagharibi kwa ajili ya kudhamini usalama wa safari za meli pia yananapaswa kuchunguzwa kwa makini, kwa sababu yanaweza kuzidisha mivutano ya sasa na kuwa mgogoro wa kimataifa.
Kuna uwezekano pia kwamba, mashambulizi haya ya kigaidi dhidi ya meli yanafanyika kwa shabaha ya kuzigonganisha na kuzitumbukiza vitani nchi za kanda hii. Mwezi Juni mwaka huu meli mbili za mafuta zilishambuliwa katika Bahari ya Oman. Vyombo vya habari na duru za kisiasa viliitaja hujuma dhidi ya meli hizo kuwa ni njama yenye lengo la kulitumbukiza vitani eneo la Ghuba ya Uajemi na kuizidishia Iran mashinikizo.
Qassim Izuddin mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Hizi ni njama za wapenda vita zenye shabaha ya kulitumbukiza tena eneo la Ghuba ya Uajemi katika vita.
Shambulio la Ijumaa dhidi ya meli ya mafuta ya Iran pia linaweza kutathminiwa kuwa ni mwendelezo wa njama za miezi iliyopita za kuzusha mivutano na kuvuruga amani katika njia nyeti za safari za meli baharini na kusababisha hali ya mvutano katika mazingira yanayoizunguka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kukariwa kwa matukio ya aina hii kutaidhuru na kuhatarisha pia dunia kwa sababu, matukio kama haya yataandaa uwanja wa kushuhudiwa ukosefu mkubwa wa amani ambao hautakuwa na manufaa kwa nchi yoyote. Uharamia wa baharini na kuzusha machafuko katika eneo la Ghuba ya Uajemi na katika maji ya kimataifa ni mchezo hatari ambao hautakuwa na mwisho mwema kwa upande wowote ule.
Kama alivyoeleza Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran: Dhima yote ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira uliosababishwa na kushambuliwa meli hiyo iko juu ya wanaofanya chokochoko kwenye eneo hili.
/129